Dar/Zanzibar.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wajumbe wa Bunge la Katiba
kutoka katika chama chake hawatashiriki katika Bunge hilo linalotarajiwa
kuendelea mwezi ujao ikiwa mambo makuu manne hayatafanyiwa marekebisho
na kuzingatiwa. Mbowe alitaja mambo hayo kuwa ni;
Kudeleza mazungumzo na Rais Kikwete kwani ndiye msimamizi mkuu wa mchakato wa Katiba.
“Kamati Kuu imebariki kuendelea kwa
mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Ukawa, pia upande wa Serikali kuhusu
namna ya kunasua mchakato huu ndani ya Bunge Maalumu. Kikao cha Sitta ni
sehemu ya Bunge la Katiba, sisi kama Chadema na Ukawa pia hatutashiriki
kikao hicho kwa sababu tunaamini kitakachojadiliwa hakitapishana na
yaliyotokea bungeni.”
Julai 8 mwaka huu, Sitta aliitisha
kikao cha wajumbe 27 wa kamati ya mashauriano wakiwamo maaskofu wawili
ili kuondoa mpasuko kati ya Ukawa na wajumbe wengine.
Alisema licha ya kuwapo mazungumzo ya kuwataka Ukawa kurejea bungeni,
CCM kimekuwa kikitumia mwanya huo ili wakirejea kiendeleze mkakati wake
wa kubadili kila jambo katika rasimu hiyo.
“Kesho (leo) tutakutana na CCM ila siwezi kukwambia ni wapi. Tunaamini
mazungumzo na Rais Kikwete ndiyo yanaweza kunusuru mchakato huu,”
alisema Mbowe.
Alisema jambo la pili, wajumbe wa Ukawa kutoka Chadema watarejea kwenye
vikao vya Bunge hilo endapo mamlaka ya Bunge la Katiba itafafanuliwa
kuwa ni kuboresha na si kuibomoa au kuifuta misingi mikuu ya rasimu
hiyo.
“Tatu, wajumbe wa Ukawa kutoka Chadema watarudi bungeni iwapo ufafanuzi
uliotajwa katika sura ya pili, utahusisha marekebisho ya Kifungu cha 25
cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba” alisema Mbowe.
Akitaja sababu ya nne, Mbowe alisema wajumbe kutoka chama hicho
hawatarejea bungeni hadi ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge hilo uliotajwa
katika sura ya 2 na 3 utakapofanyika.
“Endapo kwa sababu yoyote ile Bunge Maalumu litavunjwa kabla ya
kupitishwa Rasimu ya Katiba. Chadema kama sehemu ya Ukawa itafanya
mapambano ya kupata Katiba Mpya ya kidemokrasia kuwa sehemu kuu ya
kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015,” alisema Mbowe.
Waliojiengua Chadema
Akizungumzia viongozi wa chama hicho waliojiuzulu nyadhifa zao mkoani
Kigoma na Tabora, Mbowe alisema hao ni mamluki na wameshindwa kukifanya
chama hicho kipate wabunge wengi katika mikoa hiyo... “Kama ambavyo
mawakala wa CCM wa miaka ya nyuma hawakuathiri kukua kwa Chadema,
wasaliti na mawakala wa CCM wa sasa na wasaliti na mawakala watarajiwa
hawataweza kuathiri kukua na kujiimarisha kwa chama chetu.”
Viongozi wote wa Chadema Mkoa wa Kigoma walijivua uanachama wa chama
hicho juzi. Hao ni Mwenyekiti, Jafari Ramadhani Kasisiko, katibu wake;
Msafiri Hussein Wamalwa Malunga na Katibu wa Baraza la Wanawake, Masoud
Simba. Pia Katibu wa Chadema Mkoa wa Tabora, Athumani Balozi na
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho wa mkoa, Hussein Kundecha
nao walijiuzulu.

0 comments :
Post a Comment