“Kabla
ya kuanza mechi, kocha unatakiwa kumchukua mchezaji mmoja mmoja na
kumzungusha eneo zima la uwanja kwa dakika 30, tunafanya hivyo ili
kumjengea mchezaji hali ya kuzoea mazingira ya uwanja kabla ya kucheza,”
anasema kocha wa mpira wa kengele, Hashiru Tembo
Anasema
wachezaji hupelekwa kila sehemu ya uwanja utakaotumika kwenye mechi
hiyo, ambazo ni kwenye goli wanalotakiwa kufunga na kwenye goli lao kwa
ajili ya kuzuia na mwisho wa uwanja, pia katikati ili kung’amua urefu na
ukubwa wa uwanja watakaoutumia.
Mpira
wa kengele au ‘Goal ball’ ni mchezo ulioanzishwa na raia wa Australia,
Hanzi Lorenzen na raia wa Ujerumani, Sepp Reindle mwaka 1946 kwa ajili
ya kuwasaidia askari waliopigana vita ya pili ya dunia na kupata
matatizo ya macho.
Kwa
mara ya kwanza nchini mchezo huu umechezwa kwenye mashindano ya 20 ya
Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta)
ya msimu huu kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, Pwani.
Mpira wa kengele unavyochezwa
Hashiru
Tembo ambaye ni kocha wa mchezo huo anasema mpira wa kengele unachezwa
na wachezaji wasioona (vipofu) na wenye uoni hafifu ambao kabla ya
kuanza kwa mechi wote huvaa vitambaa vyeusi kuziba macho kwa ajili ya
kuzuia wale wenye uoni hafifu kutoona kabisa ili kuendana na wenzao
(vipofu).
Timu nzima ina wachezaji wangapi?
Tembo
anasema kila timu inasajili wachezaji wanne, ambao kati yao watatu
wanakuwa kwenye kikosi cha kwanza na mmoja anakuwa mchezaji wa akiba,
wanaoanza mmoja anakuwa mchezaji wa kati na wachezaji wawili wa pembeni.
“Mchezaji
wa kati mara nyingi anakuwa yule mwenye hisia za haraka za kubaini
mpira pale unapokuwa umerushwa golini kwao na anapoudaka hatakiwi
kuugusa zaidi ya mara mbili, akishagusa mara mbili anapaswa kumpa
mchezaji wa pembeni akigusa mara ya tatu hiyo ni faulo,” anasema Tembo.
Anasema
mchezaji wa kati ambaye ni muhimu kwa ulinzi anapougusa mpira kwa kuwa
ni mchezo wa wasioona, anapaswa kufanya ishara ya kugusa mpira kwa nguvu
kidogo ili kengele itoe sauti kumwashiria yule wa pembeni kuwa anampa
pasi.
“Akiugusa
mara ya tatu hiyo ni faulo, na faulo za mpira wa kengele ni kupigwa kwa
penati, wakati wa upigaji wa penati wachezaji wa pembeni wanapaswa
kutolewa na kubaki yule wa kati peke yake,” anasema Tembo.
Anasema
mpira wa kengele hauna kona wala mpira wa kurusha, goli linapofungwa
timu iliyofungwa ndiyo inaanzisha mpira kutoka pembeni mwa goli lao na
mchezaji atakayetoa nje mpira unapelekwa kuanzwa kwenye lango la timu
pinzani.
Washangiliaji wanaruhusiwa
“Ndiyo
washangiliaji wanaruhusiwa kwa sharti la kuwa watazamaji tu bila
kushangilia hadi pale goli litakapoingia ndipo wanaruhusiwa kupiga
makofi tena kwa sekunde chache tu na kukaa,” anasema Tembo.
Anasema mpira wa kengele hautaki kelele kwani wachezaji wanapaswa wasikie sauti ya kengele wakati mpira unaporushwa.
“Tofauti
na michezo mingine timu zinaweza kushangilia kwa mavuvuzela, ngoma,
sauti kali muda wote, lakini kwenye mpira wa kengele ni kinyume,
hakutakiwi kabisa kelele ili kuwapa fursa wachezaji kusikia kengele ya
mpira,” anasema Tembo.
Kwa nini wanachezea kwenye zulia?
Tembo
anasema uwanja wa mpira wa kengele unapaswa kuwa na zulia kwenye magoli
ya pande zote mbili ili kuwasaidia wachezaji kutopata michubuko au
majeraha wakati wa mechi.
“Mpira
wa kengele unachezwa wakati wachezaji wakiwa wamepiga magoti ili kuweza
kuusikia vizuri mpira unapokuja langoni kwao, na kawaida uwanja wa
mpira wa kengele umesakafiwa kama vilivyo viwanja vya kikapu na
netiboli.
“Tofauti
yake ni kwamba uwanja wa mpira wa kengele unakuwa na magoli kama ya
soka, lakini mafupi na mapana, hivyo kapeti linawasaidia kutoumia kwani
mbali ya kupiga magoti, mchezaji anaweza kujirusha kuelekea anaposikia
mlio wa kengele ili kuufuata mpira,” anasema Tembo.
Anasema
mbali na uwanja kuwekewa zulia, pia wachezaji wote wanapaswa kuvaa vitu
vitakavyowasaidia kutopata michubuko sehemu za magoti na kwenye viwiko
vya mikono wakati wa mechi.
Kocha anaruhusiwa kusimamisha mechi?
“Ni
kweli kocha anaruhusiwa kusimamisha mpira (mapumziko mafupi) mara tatu
katika dakika zote 24 za mechi kwani mechi huchezwa kwa dakika 12
kipindi cha kwanza na dakika 12 kipindi cha pili, akizimaliza haruhusiwi
kuomba tena,” anasema Tembo.
Anasema
mara nyingi huwa wanaomba mapumziko mafupi ili kuwaweka vizuri
wachezaji wao uwanjani ambapo kuna wakati mchezaji anaweza kuwa
amegeukia pembeni ya uwanja bila kujua wakati mechi inaendelea.
“Mchezaji
anaweza kuwa amegeukia pembeni au anaangalia nyuma ya uwanja kwa kuwa
anakuwa haoni, hivyo kocha anaweza kuomba mapumziko mafupi na kwenda
kumrekebisha na kumuweka vizuri japo mwisho wa kuomba ni mara tatu,”
anasema Tembo.
Mazoezi yao yanafanyikaje?
“Mpira
wa kengele ni mzito hivyo wachezaji wanapaswa kutumia nguvu kidogo
katika kuurusha, ili kuendana na mpira wachezaji huwa wanafanya mazoezi
makali ikiwamo ya gym, na kukimbia kwa ajili ya pumzi,” anasema Tembo.
Anasema,
wanapofanya zoezi la kukimbia, yule mwenye uoni hafifu humshika mkono
yule asiyeona kabisa na kuanza kukimbia naye kwa kuzunguka uwanja wa
mpira wa miguu raundi kadhaa au eneo lolote ambalo kocha anaona
linastahili.
Changamoto wanazokutana nazo wachezaji
Aman Fungo ni mchezaji wa mkoa wa Iringa, yeye anasema changamoto kubwa ni ukosefu wa viwanja vya mchezo huo hapa nchini.
“Mara
nyingi tunatumia viwanja vya michezo mingine, kama kwenye Umitashumta
tulikuwa tunatumia uwanja wa mpira wa kikapu ambao upo jirani na ule wa
netiboli na wavu hivyo tunapokuwa tunacheza sisi michezo mingine
inasimamishwa au tunatakiwa tucheze asubuhi sana kabla michezo mingine
haijaanza,” anasema Fungo.
Wakati
Seleman Omary wa Dodoma anasema, uhaba wa viwanja na vifaa ni
changamoto kwao kwani vinavyotumika viko katika mazingira ya kelele
ingawa mchezo huo hautaki kelele.
“Uwanja
wa mpira wa kengele unapaswa kuzungushiwa uzio ili kuzuia mpira usitoke
nje ya eneo la uwanja, lakini viwanja tunavyovitumia havina uzio na
mara nyingi tunatumia vile ambavyo ni maalumu kwa michezo mingine kwa
ujumla sisi hatuna viwanja,” anasema Omary.
Mchezo huo unavyowasaidia walemavu
Kocha
Tembo anasema tangu ulipoanzishwa mpira wa kengele, walemavu wa macho
mkoani Dodoma wamehamasika mno kucheza na umewajengea kujiamini na
kujiona hawana tofauti na jamii ya kawaida.
“Kwanza
wamejiona sio tofauti na watu wengine, wamejenga mahusiano mazuri na
wachezaji wengine, lakini pia umewasaidia kuwa wadadisi na hata maarifa
kwao yameongezeka mara dufu kulinganisha na walivyokuwa awali,” anasema
kocha huyo.

0 comments :
Post a Comment