Watafiti katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple, Marekani
wamegundua dawa ya kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambayo ni ya
uhakika zaidi ukilinganisha na zilizowahi kupatikana katika tafiti za
awali duniani.
Dawa yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili aliwaambia waandishi wa habari
juzi mjini Philadelphia, Marekani kuwa tofauti na utafiti mwingine, wao
wamegundua namna ya kukiondoa kirusi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA)
ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua.
Alisema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk Khalili alisema ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu
teknolojia ya kutengeneza dawa hiyo ni tofauti na nyingine zilizokwisha
kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa kupenya ndani ya seli za binadamu,
bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake, ndani ya mfumo wa damu.
“Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli
yenyewe na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua
virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo
dawa ya kufubaza VVU (ARV).”
ARV huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kuendelea kuviacha hai vile
ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4, hivyo kufanya virusi kuzuka upya
pindi mwathirika anapoacha kutumia dawa.
Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani ameuelezea utafiti
huo kama mwanga mpya katika teknolojia ya kukabili VVU.
“Kama imepatikana teknolojia ya kukiondoa kirusi ndani ya seli ni
hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili lilionekana kuwa gumu mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi
ya wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli
zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo likawa gumu.
“Inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika)
lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili. Hilo halikubaliki.
Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata kirusi
kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa
zikiwamo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.
“Lazima dawa hiyo ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine
pamoja na utendaji wa mwili kwa ujumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi
zinaposhindwa… Tusubiri tuone hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,” alisema Majani.
Mkutano wa Ukimwi
Ugunduzi huo umekuja wakati wanasayansi, waunda sera na wadau wa
mapambano ya VVU wakiwa wanatoa kauli za kukata tamaa kwenye mkutano wa
Ukimwi unaomalizika kesho huko Melbourne, Australia.
Wanasayansi kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za utafiti za VVU
wameweka wazi kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa
kufanya kazi kwa asilimia 100 baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio kwa
sababu dawa zake zinapotumika, vipimo huonyesha wamepona lakini baada
ya muda VVU hurejea upya.
“Kinachoonekana ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya
mwili ili visiathirike na kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya
kushambulia CD4,” alisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya wa
Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty ya Australia, Profesa
Sharon Lewin.
Dawa mpya inavyofanya kazi
Dk Khalili alisema wametengeneza dawa yao kwa protini maalumu ambayo
inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta
nje.
Baada ya kukivuta, dawa huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu
yenyewe na kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga
mwilini mwa binadamu bila tatizo.
VVU kwa kawaida hushambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama kiwanda cha kuzalishia virusi vingine.
Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi, huacha kazi yake ya kinga ya
mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
“Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kwa makini na bila kuathiri seli,” alijigamba Dk Khalili.
Alisema tayari imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama.
Katika maabara, alisema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100.
Dk Khalili anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache...
“Lakini tunaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa binadamu.” Alisema wanachofanya sasa ni kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya tiba ya binadamu.
Kwa namna teknolojia ya dawa hiyo ilivyo, alisema wanaweza kuitumia kwa
ajili ya kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa na hata kuwakinga wale
ambao siyo waathirika.
Uzuri wa dawa hiyo, pia alisema inaweza kutumiwa na mtu ambaye anatumia ARV pasipo kuingiliana kiutendaji.
Ugunduzi wao ulichapishwa kwenye Jarida la Taifa la Elimu ya Sayansi la
National Academy of Science la Marekani na kuonekana kuvuta hisia za
wengi.
Hali ya Ukimwi duniani
Akizungumza kwenye mkutano wa Melbourne, Profesa Lewin alisema tafiti za
sasa zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 14 duniani wanaishi na VVU.
Alisema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambao bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.
Alisema ingawa tafiti nyingi hazijaonyesha matumaini waliotarajia ya
kupata kinga na chanjo, bado juhudi zinaendelea ili kuhakikisha
wanafikia mahali HIV inakuwa haina nafasi katika mwili wa mwanadamu.
Alisema pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi,
bado anaamini kwamba ipo siku chanjo na tiba vitapatikana.
Wanasayansi waliohudhuria mkutano huo waliitaka dunia isiogope kutokana
na kushindwa kwa baadhi ya tafiti kama ilivyokuwa kwa mtoto wa Jimbo la
Mississippi, nchini Marekani ambaye alitangazwa amepona na baadaye
virusi vikaibuka upya.

0 comments :
Post a Comment